MTWANGAJI
01:Nianze na wa nyumbani, salamu kuwatolea
Jamani mu hali gani, zipoje zenu afia
Nanyi wa ughaibuni, amani nawatakia
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
02:Niwajuze yangu fani, kwa dhati nilobobea
Si fundi wa cherehani, dereva na abiria
Wala ticha darasani, zote sijazizoea
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
03:Si nguvu bali akili, ndio ninayotumia
Kinu ninakikabili, mtwangio kushushia
Mimi fundi kwelikweli, kutwanga nimebobea
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
04:Nikiziona nafaka, zimetulia kinuni
Unanipanda wahaka, nasisimuka mwilini
Mchi mate naupaka, tayari nipo kazini
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
05:Tena kutwangia kinu, kisikalie pembeni
Zisije kufeli mbinu, mchi ukatwanga chini
Kina mwajuma na tunu, wanione punguani
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
06:Ukitua mtwangio, kusaga hizo nafaka
Hubakia mshangao, kinu kina taabika
Nakaa kila mkao, ufaao kutwangika
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
07:Umakini naongeza, ninapotwanga kinuni
Natwanga na kupuliza, kwa kati na ukingoni
Nafaka zisijecheza, nikamwagia pembeni
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
08:Ya utwanzi kazi yangu, siifanyi
hadharani
Mimi sifinyangi chungu, kwamba nikae juani
Najificha ndani kwangu, nafaka natwanga
ndani
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
09:Tam tam yangu kazi, mwenyewe nimeridhika
Nahema kwa kasi pumzi, ninapoanza kuchoka
Ninatwanga kwa mapozi, kijasho kikinitoka
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
10:Zinapoiva nafaka, mtwangio nautoa
Kinu maji nakipaka, kesho nije kitumia
Moyoni nafurahika, kazi imeshatimia
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
11:Kufanya nyengine kazi, hilo wazo na
likome
Sibadili maamuzi, wacha roho ziwaume
Nitazidisha ujuzi, najiamini kidume
Naringia mtwangio, unaniweka mjini.
MTUNZI:HUSSEIN.R.KAPARATA
TEL:0714631510
huseinkapa112@gmail.com

Comments
Post a Comment