Skip to main content

 

          BWANA DHIKI



1;Hana baba wala mama,wala ndugu wa kunusa

Halali ndani ya hema,jua mvua yamtosa

Ngozi yake ya ukoma,ngumu kwa kuipapasa

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

2;Hana kazi wala bazi,anafanya dei waka

Elimu hana ujuzi,darasani hakufika

Machinga na wachuuzi,humfanya kibaraka

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

3;Kuu kuu nguo zake,mabwende yalotoboka

Waume kwa wanawake,husema amechizika

Upitapo kando yake,uvundo unamnuka

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

4;Sura yake ni nyeusi,tii yenye kupauka

Mfupi kama kipisi,ama shina la mugoka

Mapele kama fenesi,ngoziye imebabuka

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

5;Watupavyo jalalani,vyote vilo haribika

Ndizi mboga za majani,na nyama zinazo nuka

Hushindilia tumboni,haogopi kudhurika

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.


6;Yupo peku miguuni,kokoto zinamng'ata

Apitapo jalalani,vigae vinamsuta

Augulia rohoni,maumivu anopata

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

7;Mwanzo alilia sana,hadi kwikwi kumtoka

Sasa ametulizana,machozi yamekauka

Wakumjali hakuna,lau angeimarika

Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.

 

8;Macho wamemfumbia,wenye vikubwa vitambi

Viziwi wanajitia,wazidisha na vitimbi

Eti ameyazoea,maisha ya kula vumbi!

Utu wa mtu ni utu,musiupime kwa kitu.

 

9;Kwa fujo wanampita,ndani ya yao magari

Wazidi kukunja ndita,kwake hawana habari

Watupacho aokota,mola kampa nusuri

Utu wa mtu ni utu,musiupime kwa kitu.

 

10;Angalikuwa na baba,ama japo familia

Asinge pata suluba,nafuu ingemjia

Dunia inamkaba,hana wa kumtetea,

Utu wa mtu ni utu, musiupime kwa kitu.

 

11;Kaparata najivika,joho la kumtetea

Nahisi hapa patosha,mkome kumkandia

Kula kwa kurasha rasha,ni dhiki hakuzoea

Utu wa mtu ni utu,musiupime kwa kitu.

 

12;Zifikisheni habari,kwa mandusa na vitambi

Wasijipe ujabari,wa kuhalalisha dhambi

Wakanye kwa tahadhari,vikome vyao vitimbi

Utu wa mtu ni utu,musiupime kwa kitu.

 

13;Kama kuandika sumu,adhabu inikabili

Silaha yangu kalamu,kuondosha idhilali

Sababu yalo haramu,kuyaacha ni muhali

Utu wa mtu ni utu,musiupime kwa kitu.



                 *MWISHO*

 Mtunzi:Hussien.R.Kaparata

TEL.0714631510

Comments

Popular posts from this blog

      MTWANGAJI 01:Nianze na wa nyumbani, salamu kuwatolea Jamani mu hali gani, zipoje zenu afia Nanyi wa ughaibuni, amani nawatakia Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   02:Niwajuze yangu fani, kwa dhati nilobobea Si fundi wa cherehani, dereva na abiria Wala ticha darasani, zote sijazizoea Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   03:Si nguvu bali akili, ndio ninayotumia Kinu ninakikabili, mtwangio kushushia Mimi fundi kwelikweli, kutwanga nimebobea Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   04:Nikiziona nafaka, zimetulia kinuni Unanipanda wahaka, nasisimuka mwilini Mchi mate naupaka, tayari nipo kazini Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   05:Tena kutwangia kinu, kisikalie pembeni Zisije kufeli mbinu, mchi ukatwanga chini Kina mwajuma na tunu, wanione punguani Naringia mtwangio, unaniweka mjini. 06:Ukitua mtwangio, kusaga hizo nafaka Hubakia mshangao, kinu kina taabika Nakaa kila mkao, ufaao kutwangika Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   07:Umakini na...
                    MLAJI 1;Enyi walaji wa leyo, kusema nanyi nataka Ipunguzeni pupiyo, lasivyo mtadhurika Nyoyo zipeni zuiyo, mwili utabusarika Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.   2;Mnapopita shambani, matunda yawazuzuwa Mboga hamzitamani, zawachosha kuchambuwa Macho yote yamtini, paku mnaupekuwa Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.   3;Muonapo tunda pera, limelala kidarini Nyanyachungu ama tura, mbili mbili zi tawini Kwa kebehi mnafura, mwasema hizi za nini Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.   4;Mwataka ulojazia, mti hadi mashinani Ili ukiupandia, uhisi u kitandani Huku dodo wajilia, wajipea burudani Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.   5;Muonapo ni papai, au dodo mwalichuma Mwajitia ubedui, kulipapasa kwa nyuma Kifuatacho jimai, kichwani mwawaza nyama Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.   6;Kisha hufata vurugu, za kwichi kwichi mtini Yale mavuno ya njugu, mli...