Skip to main content

                   MLAJI



1;Enyi walaji wa leyo, kusema nanyi nataka

Ipunguzeni pupiyo, lasivyo mtadhurika

Nyoyo zipeni zuiyo, mwili utabusarika

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

2;Mnapopita shambani, matunda yawazuzuwa

Mboga hamzitamani, zawachosha kuchambuwa

Macho yote yamtini, paku mnaupekuwa

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

3;Muonapo tunda pera, limelala kidarini

Nyanyachungu ama tura, mbili mbili zi tawini

Kwa kebehi mnafura, mwasema hizi za nini

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

4;Mwataka ulojazia, mti hadi mashinani

Ili ukiupandia, uhisi u kitandani

Huku dodo wajilia, wajipea burudani

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

5;Muonapo ni papai, au dodo mwalichuma

Mwajitia ubedui, kulipapasa kwa nyuma

Kifuatacho jimai, kichwani mwawaza nyama

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

6;Kisha hufata vurugu, za kwichi kwichi mtini

Yale mavuno ya njugu, mlizokula shambani

Leo mwazimwaga mbegu, kwa mineso matawini

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia

 

7;Ladha ya tunda nanasi, madodo ama balungi

Haipimwi kwa nafasi, ama kujazia vingi

Maviru yana virusi, iogopeni mitungi

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

8;Najua shida ni moyo, walaji mwataabika

Mwashindwa weka zuiyo, kula vilo sitirika

Mwafulani shauriyo, mauti yatakufika

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

9;Alisema muandishi, tamayo kuihusudu

Kwa hati ya maandishi, madodo yana wadudu

Msitilie ubishi, ama takufa kibudu

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.

 

10;Tama Aisha Johari, tembeeni na pakacha

Imechafuka bahari, refarii kawa kocha

Msivimbishe vidari, mtageuzwa chamcha

Shikilia wako moyo, mlaji utaumia.



            *MWISHO*

Mtunzi: Husein.R.Kaparata

         TEL.0714631510

Email.huseinkapa112@gmail.com

 


Comments

Popular posts from this blog

      MTWANGAJI 01:Nianze na wa nyumbani, salamu kuwatolea Jamani mu hali gani, zipoje zenu afia Nanyi wa ughaibuni, amani nawatakia Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   02:Niwajuze yangu fani, kwa dhati nilobobea Si fundi wa cherehani, dereva na abiria Wala ticha darasani, zote sijazizoea Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   03:Si nguvu bali akili, ndio ninayotumia Kinu ninakikabili, mtwangio kushushia Mimi fundi kwelikweli, kutwanga nimebobea Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   04:Nikiziona nafaka, zimetulia kinuni Unanipanda wahaka, nasisimuka mwilini Mchi mate naupaka, tayari nipo kazini Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   05:Tena kutwangia kinu, kisikalie pembeni Zisije kufeli mbinu, mchi ukatwanga chini Kina mwajuma na tunu, wanione punguani Naringia mtwangio, unaniweka mjini. 06:Ukitua mtwangio, kusaga hizo nafaka Hubakia mshangao, kinu kina taabika Nakaa kila mkao, ufaao kutwangika Naringia mtwangio, unaniweka mjini.   07:Umakini na...
            BWANA DHIKI 1;Hana baba wala mama,wala ndugu wa kunusa Halali ndani ya hema,jua mvua yamtosa Ngozi yake ya ukoma,ngumu kwa kuipapasa Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.   2;Hana kazi wala bazi,anafanya dei waka Elimu hana ujuzi,darasani hakufika Machinga na wachuuzi,humfanya kibaraka Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.   3;Kuu kuu nguo zake,mabwende yalotoboka Waume kwa wanawake,husema amechizika Upitapo kando yake,uvundo unamnuka Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.   4;Sura yake ni nyeusi,tii yenye kupauka Mfupi kama kipisi,ama shina la mugoka Mapele kama fenesi,ngoziye imebabuka Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha.   5;Watupavyo jalalani,vyote vilo haribika Ndizi mboga za majani,na nyama zinazo nuka Hushindilia tumboni,haogopi kudhurika Wamuita bwana dhiki,jinale yake maisha. 6;Yupo peku miguuni,kokoto zinamng'ata Apitapo jalalani,vigae v...